Masista wa UrsulaESPANSIONE-descrizione in lingua italianawa Tanzania

 

Mtakatifu Anjela Merici (1474 – 1540)


 

Mt. Anjela alizaliwa katika kijiji cha Desenzano karibu na Brescia huko Italia ya kaskazini- mnamo mwaka 1474. Alizaliwa katika familia ya kikristo ambayo ilikuwa si tajiri wala si maskini. Yeye alikuwa mtoto wa tano katika familia ya watoto sita. Baba yake alipenda kuwasomea watu wa familia yake historia za watakatifu. Historia hizo zilijenga moyoni mwa Anjela upendo kwa Yesu na ibada na heshima kwa mtakatifu Ursula. Baba yake Anjela ambaye aliitwa Yohana alikuwa mkulima. Mama yake aliitwa Catherine na alikuwa na kaka yake ambaye alikuwa mmoja kati ya watu wa Halmashauri ya mji wa Salò karibu na Brescia. Anjela alikuwa na kaka wanne na dada mmoja. Aliishi Desenzano kipindi chote cha ujana wake katika sehemu iliyoitwa “Grezze”. Anjela alipata malezi bora ya kiroho kutoka kwa wazazi wake.

Alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitano (15) Anjela alifiwa na wazazi wake wote wawili na alilazimishwa kwenda kuishi huko Salò kwa mjomba wake pamoja na dada yake. Nyumba ya mjomba wake ilikuwa mahali ambapo Anjela angeweza kuwasiliana na watu mbalimbali wenye elimu, kwa hiyo Anjela alijifunza kusoma lakini hakujifunza kuandika. Ni kwa sababu hiyo katika maisha yake hakuweza kuandika, hivyo daima alimtumia karani wake, kufanya kazi ya kuandika.

Huko Salò alianza kuishi maisha ya toba akipigana na maadili mabaya ya watu wa mazingira alimoishi.

Wakati huo alifanya uamuzi wake wa kwanza wa maisha: kuwa mtawa wa utawa wa tatu wa Wafransisco ili kumfuata Kristo kwa ukaribu zaidi na pia ili aweze kupokea kwa uhuru zaidi sakramenti ya Kitubio na Ekaristi. Kuanzia wakati ule watu wote walianza kumwita Sista Anjela.

Alipofikisha umri wa miaka ishirini (20), mjomba wake alifariki, Anjela alirudi tena kijijini kwao Desenzano, kwa lengo la kuamua kwa uhuru zaidi kuhusu maisha yake. Huko Desenzano yeye alikuwa na shamba ambalo alipata kama urithi kutoka kwa wazazi wake, alianza kulima shamba na kuishi maisha ya kazi, sala na matendo ya huruma. Wakati ule ule, wito ulikomaa ndani yake.

Mwaka 1506 (akiwa na miaka 32) aliona maono: Alikuwa shambani akizama katika sala na huko aliona mbingu zikifunguka na malaika walishuka kutoka mbinguni wakiwa pamoja na mabikira wengi.

Mwaka 1516 alipokuwa na umri wa miaka 40 alihamia mjini Brescia alikuwa akiishi maisha ya ufukara na sala. Watu wengi, hata maaskofu na makardinali, walikuwa wakienda kwake ili kuomba ushauri wa kiroho. Wakati huo alianza utume wake wa kuwafariji, kuwashauri, kuwapatanisha watu na kusali kwa ajili ya wote ambao waliomba msaada wake.

Mara kwa mara alifikiri ni kwa namna gani angeweza kutumia maisha yake: kwa njia ya sala na tafakari alielewa kwamba konventi sio kwa ajili yake …

Basi ili kupata msaada wa kutambua wito wa maisha yake alianza kufanya hija mbalimbali.

Tangu zamani hija husaidia kupata uongovu wa ndani, na maana yake hasa ni “watu wanaotembea ili kumtafuta Kristo

Alikuwa akifanya hija mbalimbali lakini hija ya muhimu katika maisha yake ya kiroho ilikuwa ni ile hija aliyohiji katika Nchi ya Yesu mwaka 1524. Kabla ya kufika Nchi ya Yesu kulitokea aina fulani ya muujiza: Anjela alipoteza uwezo wake wa kuona kwa hiyo alifika Nchi ya Yesu lakini hakuiona.

Anjela mwenyewe alisema kwamba Mungu alimfanya awe kipofu ili aweze kuona sehemu mbalimbali alizoishi Yesu, kwa macho ya kiroho. Aliporudi Italia alianza kuona tena.

Safari yake katika nchi ya Yesu ilimbadilisha kabisa na mabadiliko hayo yalikuwa yakionekana katika mwili wa Anjela, kwa hiyo wote walitambua kwamba Anjela ni Mtakatifu na wengi walienda kumtembelea ili kupata msaada.

Mwaka 1525 alienda hija Roma ili kufanya jubilei na alipata ruhusa ya kukutana na Baba Mtakatifu Clemente VII ambaye alivutiwa na karama yake na alimwomba abaki huko Roma ili afanye kazi huko. Lakini Anjela alikataa kwa sababu alimsikia Roho Mtakatifu akimwita kufanya kazi sehemu nyingine. Baba Mtakatifu alimwelewa na yeye alirudi Brescia.

Aliporudi mjini Brescia, akiwa na miaka hamsini, hakuwa tena mama yule aliyeanza kufanya hija miaka kumi iliyopita. Safari zake hizo za hija zilimbadilisha. Maisha yake ya kiroho yakawa ya ndani kabisa. Aliweza kuelewa maana ya kiroho ya mambo mbalimbali na akawa na hekima.

Wote wanautambua utakatifu wake.

Kwa njia ya maono Anjela alipata wazo la kuanzisha Shirika la wasichana mabikira. Katika maono hayo aliona ngazi ndefu iliyounganisha mbingu na dunia na kwenye ngazi hiyo aliona wasichana wengi wakipanda ngazi, kila mmoja akielekea kwa malaika wake mlinzi. Katika wasichana hao alimfahamu msichana mmoja ambaye alikuwa rafiki yake aliyefariki. Huyu rafiki yake alimwambia aanzishe Shirika kwa lengo la kuwalea wasichana. Kwa njia ya maono hayo, Anjela alielewa jambo ambalo Mungu alilitaka kwake, jambo hilo lilikuwa ni kuanzisha Shirika ili awasaidie wasichana. Na alifanya hivyo.

Anjela alipofikisha umri wa miaka 60 akiwa tajiri wa fadhila na mjuzi wa mambo ya kiroho, aliwaza kuwaelekeza hata wanawake wengine namna yeye alivyopenda kuishi katika sala, kutafakari na kutenda matendo ya huruma. Mwaka 1529 alihamia Brescia na aliwaambia kikundi cha akina mama marafiki zake kwamba alikuwa ameweka nadhiri kwa siri na alijiweka wakfu kwa Kristo na pia kwamba alimwahidi Kristo kumtumikia katika jirani hasa katika wasichana wale ambao walikuwa wakihitaji zaidi msaada, huduma na upendo.

Karama ya Anjela iliwavutia marafiki zake na kati yao kumi na wawili waliamua kumfuata kutoka maeneo mbalimbali, wakijiweka wakfu kwa Kristo, pasipo kukaa konventini na pasipo kuvaa nguo za kitawa bali kila mmoja aliishi nyumbani kwake na aliendelea na kazi zake za kawaida na kwa namna hiyo waliweza kuwa huru zaidi kuwasaidia jirani: wagonjwa, wajane, wasichana yatima, kufundisha katekisimu kwa watoto, kufanya usafi kanisani n.k.

Anjela alimchagua Kristo kama nguzo ya maisha yake. Yeye alijiweka wakfu kwake kwa upendo wa pekee, alimpenda kwa upendo mkubwa, kwa sababu Kristo alikuwa mchumba wake.

Haya yalikuwa mapinduzi makubwa katika kanisa:

Wa-Ursula

Kwa nini shirika linaitwa la Mt. Ursula?

Anjela tangu utoto wake, wakati baba yake alipokuwa akiwasomea historia za watakatifu mbalimbali, yeye alimpenda sana Ursula, msichana, mwana wa mfalme wa Uingereza ambaye aliwaambia wasichana marafiki zake siri yake ya kujiweka wakfu kwa Kristo na kutaka kuwa mwaminifu kwake tu (alikuwa akikataa kuolewa na mfalme mmoja mpagani). Wale wasichana marafiki zake walikuwa wapagani lakini walipopata mafundisho kutoka kwa Ursula walifuata mfano wake hadi kufa kifodini huko Ujerumani na kubaki waaminifu kwa Kristo. Anjela alivutiwa sana na historia ya Ursula na wenzake na alitaka ujasiri wa kupokea safari yenye shida mbalimbali na kifodini uwe hata ujasiri wa wasichana wa Shirika lake. Anjela alimchagua Mt. Ursula awe msimamizi wa Shirika lake.

Hali ya wanawake duniani katika karne “16”

Wakati huo wanawake walitakiwa ama kuolewa au kuingia katika konventi ya klausura. Ni familia yake ndiyo iliyokuwa na uamuzi juu ya maisha ya msichana. Anjela alitamani kujiweka wakfu kwa Mungu lakini sio kuishi ndani ya konventi bali kujiweka wakfu katikati ya jamii, ili aweze kugundua haraka zaidi mahitaji ya kiroho na ya kimwili ya watu. Wakati wa Anjela konventi za wanawake zilikuwa 11 zenye masista 3000. Mara nyingi katika konventi waliishi wasichana wale waliotoka katika familia tajiri ambao hawakuweza kuolewa.

Kwa njia ya Shirika la Wa-Ursula kunaanzishwa njia nyingine ya kuishi maisha ya wakfu: yaani mabikira ambao wanajiweka wakfu katika ulimwengu.

Tarehe 25 novemba 1535, kumbukumbu ya Mt Catherina wa Alessandria Mmisri, Anjela Merici alianzisha rasmi Shirika la Mt. Ursula.

Mwaka 1537 mwezi wa tatu Anjela aliteuliwa kuwa Mama Mkuu wa Shirika kwa maisha yake yote.

Anjela alifariki dunia tarehe 27 januari 1540.

Anjela alipofariki alikuwa na wafuasi 150. Baada ya kifo chake maiti iliachwa mwezi mmoja bila kuzikwa ili watu waiheshimu maiti yake na haikuharibika.

Alitangazwa mwenye heri tarehe 30 april 1768 na alitangazwa Mtakatifu tarehe 24 mei 1807.

Anjela baada ya kifo chake amewaachia sio tu watoto wake bali hata walezi wote utaratibu wake wa malezi uliofanyika hasa kwa upendo wa kweli kwa walelewa na kuheshimu uhuru wao. Ameacha pia ndani ya Kanisa mfano angavu wa mtu jasiri, mwenye ubunifu ambaye aliwapenda na kuwasaidia wasichana wa wakati wake, hasa wale waliohitaji sana msaada wa kiroho na kimwili. Yeye alitenda daima kwa sababu alisukumwa na upendo wa pekee kwa ajili ya Yesu.