Masista wa UrsulaESPANSIONE-descrizione in lingua italianawa Tanzania

 

"Maisha ya Mt. Ursula" - p. Richard Mjigwa CPPS


Mtakatifu Ursula 1865-1939

    Jubilee ya miaka 150 tangu alipozaliwa

    Jubilee ya miaka 150 ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Ursula, mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Ursula wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Mteswa.

Shirika la Masista wa Ursula wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Mteswa, maarufu kama "Masista wa Mkiwa", linaadhimisha Jubilee ya miaka 150 tangu alipozaliwa Mtakatifu Ursula, aliyetangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II kunako tarehe 18 Mei 2003. Masista wa Ursula pia wanaadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu walipowasili nchini Tanzania na kukita maisha na utume wao kwa mara ya kwanza Jimboni Singida. Leo hii watawa wa Ursula wameenea katika majimbo mbali mbali nchini Tanzania. Matukio yote haya ni kielelezo cha neema na baraka za Mungu kwani Kanisa pia linaadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani na tayari kuanza maadhimisho ya Jubilee kuu ya huruma ya Mungu.

Giulia Ledochowska, aliyezaliwa kunako 17 Aprili 1865 huko Loosdorf, Austria akabahatika kukua na kulelewa katika familia bora ya Kikristo, iliyohakikisha kwamba, watoto wao saba wanafundwa katika maisha ya kiroho, kimwili, kiutu na kimaadili. Walifundishwa kuonja shida na mahangaiko ya jirani zao hasa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Giulia alijiona kuwa kama mwanga angavu kati ya maskini na kwa njia hii alionja pia uwepo wa Mungu katika maisha yake.

Akiwa na umri wa miaka ishirini na moja, Giulia akamfunulia Mama yake mpango uliokuwa umefichika moyoni mwake, kwani alitamani kuacha yote na kumfuasa Yesu Kristo aliyetundikwa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa na kumwonesha mwanadamu huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Huu ndio upendo aliotaka kuumwilisha kwa njia ya utume na maisha ya kimissionari, ili watu wengi zaidi waweze kuguswa na upendo pamoja na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo mteswa.

Giulia Ledochowska kama alivyojulikana na wengi, aliweza kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake, akaona mateso na mahangaiko ya binadamu yaliyofumbatwa katika mateso na kifo cha Yesu Kristo Msalabani, kielelezo cha hali ya juu cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Giulia alionesha karama na fadhila mbali mbali katika maisha ya ujana wake: alikuwa ni kijana aliyejaliwa paji la akili na afya maridhawa, kiasi cha kusikia upendo wa Mungu ukifukuta ndani ya moyo wake.

Aliguswa na mateso ya Kristo Msalabani, akasikitishwa sana jinsi maskini walivyokuwa wanateseka na kudhalilishwa utu na heshima yao. Kwa njia ya tafakari hii, akapenda kujenga na kuimarisha urafiki wa dhati na Mwenyezi Mungu, ili aweze kujipatia msamaha wa dhambi na kuwamegea wengine ile furaha ya Kristo Msulubiwa, kwa njia ya maisha ya kitawa. Akajiunga na Shirika la Watawa wa Ursula, Jimbo kuu la Cracovia nchini Poland na kupewa jina la Ursula.

Ursula alikuwa ni mwanamke wa shoka, aliyejisadaka kwa ajili ya kuwaelimisha wanawake wakimbizi kutoka Poland waliokuwa wanaishi nchini Russia; akawahudumia maskini wa Finland bila kuchoka, akatafsiri Katekisimu, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa kwa watu aliokuwa anawahudumia, daima akijitahidi kuiona ile sura ya Kristo mteswa kati ya watu wake. Akafukuzwa kutoka Russia kwa sababu za kisiasa na kuhamia nchini Sweden, huko akajikabidhi

mikononi mwa Mwenyezi Mungu na hapo akaanza kuwahudumia wanawake waliokuwa wanateseka kutokana na madhara ya vita kuu ya kwanza ya dunia.

Vita ilisababisha majanga makubwa nchini Poland, Mama Ursula akajifunga kibwebwe na kupata ruhusa kwa viongozi wa Kanisa ili kutafuta msaada kwa ajili ya kuwahudumia wahanga wa vita kuu ya kwanza ya dunia. Hali ya hewa kisiasa ikaendelea kuchafuka zaidi, watawa waliokuwa wamebaki nchini Russia wakalazimika kufunga vilago na kuungana na Mama Ursula.

Ulikuwa ni mpango wa Mungu uliokuwa umefichika machoni pa wengi. Kunako mwaka 1920 Mama Ursula akarejea tena nchini Poland, akataka kujiunga tena na Shirika lake, lakini akawekewa kizingiti kwa kisingizio kwamba, utume uliokuwa unafanywa na Mama Ursula haukuendana na karama ya Shirika la Maista wa Ursula, Jimbo kuu la Cracovia. Akapewa masharti ya kurejea Shirikani peke yake bila ya kuwa na watawa waliokuwa wamejiunga naye wala watoto yatima aliokuwa anawahudumia. Hakukubaliana na maamuzi haya. Haikuwa rahisi kwake baada ya kukaa shirikani kwa takribani miaka 21 yaani kuanzia mwaka 1886 hadi mwaka 1907, lakini akaamua kusoma alama za nyakati na kukubaliana na mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Tarehe 7 Juni 1920 Mama Ursula akaruhusiwa kuanzisha nyumba ya kitawa, akaandika Katiba ya Shirika na kuiweka chini ya ulinzi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Mteswa. Akajikita katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina uliokuwa unagusa mahitaji ya wasichana katika masuala ya elimu na dini kwa wakulima na wafanyakazi. Kunako mwaka 1930 Kanisa likaridhia uwepo wa Shirika la Masista wa Ursula wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Mteswa. Akawataka watawa wake kujishikamanisha na huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni watawa wanaosimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Mama Ursula ni mwanamke aliyejitahidi kusoma alama za nyakati kwa Karne ya ishirini, akafuata ushauri kutoka kwa Mtakatifu Anjela Merici, muasisi wa Mashirika yote ya Waursula duniani, akajitoa bila ya kujibakiza kwa wote waliokuwa wanataka kuonja huruma na upendo wa Mungu; akawaangia mwanga wa imani na kuwafariji kwa upendo wa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Mama Ursula alitekeleza utume wake katika mazingira magumu ya kisiasa na kiuchumi, lakini hakukata tamaa, akaonesha ile furaha inayobubujika kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake. Akawataka watawa wake daima kusoma alama za nyakati na kujibu mahitaji ya Kanisa, lakini zaidi miongoni mwa maskini, kwani maskini ni nguzo madhubuti katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa maneno mengine, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji. Huduma hii itolewe kwa moyo wa unyenyekevu unaojikita katika ushuhuda wa maisha. Watawa wake wajisadake kwa ajili ya kufundisha Katekesi pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi na waamini walei ili kuyatakatifuza malimwengu. Wajitahidi kuchapa kazi, ili kupata mahitaji yao msingi. Hadi Mama Ursula alipokuwa anafariki dunia kulikuwa na Jumuiya 35 zilizokuwa na watawa 700, waliokuwa wanawahudumia maskini kwa moyo wa huruma na upendo. Leo hii kuna jumuiya 110. Watawa Ursula wanafanya utume wao katika nchi 14 na Barani Afrika wako nchini Tanzania.

Masista wa Ursula wako mstari wa mbele katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya roho na mwili. Wanapenda kuwahamasisha waamini kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa kushiriki kikamilifu katika tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji.

Itakumbukwa kwamba, Tasaufi ya Shirika la Masista wa Ursula wa Moyo Mtakatifu wa Yesu mteswa inajikita katika tafakari ya mateso ya Kristo, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni watawa wanaopaswa kuendelea kusikiliza kilio cha Yesu Msalabani, kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa njia ya Ibada kwa Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; Mashauri ya Kiinjili yanayomwilishwa katika huduma makini katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuonesha Ibada kwa Bikira Maria, kielelezo makini cha huduma na upendo katika hali ya ukimya.

Kazi kwa watawa wa Ursula ni matunda ya muungano wa kweli na Mwenyezi Mungu unaojikita katika maisha ya sala na tafakari ya kina na kwamba sala ni msingi wa maisha ya ndani kwa watawa wa Ursula. Ni watawa wanaopaswa kuonesha: utulivu, tabasamu na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye amemtoa Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo ili aweze kuteswa, kufa na kufufuka kutoka kwa wafu. Kwa njia ya matendo mema na adili, watu wapate fursa ya kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Mama Ursula alifariki dunia tarehe 29 Mei 1939 akiwa mjini Roma. Mara tu baada ya kifo chake, mchakato wa kumtangaza kuwa ni Mwenyeheri ulianza rasmi. Kunako mwaka 1959 mwili wake ulifukuliwa na kuhifadhiwa kwenye nyumba mama iliyoko mjini Roma, mahali ambapo hata Papa Yohane Paulo II alibahatika kwenda na kusali kwenye kaburi lake. Tarehe 20 Juni 1983 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Yohane Paulo II. Tarehe 15 Mei 1989 mwili wa Mwenyeheri Ursula ulipelekwa nchini Poland. Tarehe 18 Mei 2003 akatangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II akamwandika kwenye Orodha ya Watakatifu wa Kanisa, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mbele ya umati mkubwa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Jubilee ya miaka 150 tangu alipozaliwa Mtakatifu Ursula ni kipindi cha furaha na shukrani mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake.

P. Richard Mjigwa CPPS